Wednesday, August 19, 2015
True value Media:UZINDUZI WA HUDUMA MPYA YA BIMA YA MAGARI, PIKIPIKI NA BAJAJ
Ofisa Mtendaji Mkuu wa NIKO Insurance, Mannaseh Kawoloka (katikati)
akizungumza jambo katika uzinduzi wa huduma mpya ya bima ya magari, pikipiki na
bajaj inayoendeshwa na Taasisi ya Bayport Financial Services. Huduma hiyo
imezinduliwa jijini Dar es Salaam jana. Kulia ni Mratibu wa bima hiyo, Ruth
Buran na Meneja Oparesheni wa Bayport, Charles Mgeta.
Na Ismail Mang'ola
Dar es Salaam
TAASISI ya Kifedha ya Bayport Financial Services inayojihusisha na mambo ya
mikopo, imezindua huduma mpya ya bima ya magari, pikipiki na bajaj, ikiwa na
lengo la kurahisisha masuala ya usafiri kwa wateja wao ili kukwamua zaidi.
Kuanzishwa kwa huduma hiyo mpya kumetajwa kuwa kutachangia kwa kiasi kikubwa
wamiliki wa vyombo hivyo vya usafiri waliokuwa wakishindwa kulipa bima kwa
wakati na wakati mwingine mteja kupata ajali hali ya kuwa hana huduma ya bima
inayoweza kumlinda.
Akizungumza jana jijini Dar es Salaam, Mratibu wa Bima hiyo kutoka Bayport
Financial Services, Ruth Bura, alisema huduma yao wanayoshirikiana na NIKO
Insurance ina lengo kubwa la kumrudisha mteja wao (mkata bima), katika hali
aliyokuwa nayo kabla ya kupata ajali hiyo.
Alisema mara kadhaa baadhi ya Watanzania wamekuwa wakikimbizana na askari wa
usalama barabarani kwa sababu hawana bima kwenye vyombo vyao vya usafiri, ila
kwa kupitia huduma yao mpya, sasa kila mtu anaweza kujiunga na bima kwa njia
rahisi, wakiamini kuwa ni sehemu yao ya kuhakikisha wateja wao wanakuwa kwenye
usalama ili watimize wajibu wao kufanya kazi na kukuza uchumi wao na wa
Tanzania kwa ujumla.
“Ili mtu aweze kujiunga na huduma yetu ya Bima kutoka Bayport Financial
Services, kwanza anatakiwa kujaza fomu yetu ya mkopo na ile fomu ya udhibitisho
wa bima, bila kusahau nyaraka za umiliki wa gari lake ili tujiridhishe na
umiliki wake.
“Baada ya hapo, gari lake litapigwa picha tano kila pembe, ikiwa ni nyuma na
mbele na kwenye injini na tukimaliza hatua hiyo, mteja wetu atapatiwa mkataba
wa bima pamoja na ‘sticker’ kuonyesha kuwa yupo kwenye bima, huku huduma hiyo
ikiwa ni rahisi kwa sababu gharama za bima kwa mwaka ni kuanzia Sh 354,000
pamoja na VAT,” Alisema.
Naye Meneja Uendelezaji wa Biashara wa NIKO Insurance, Jabir Kigoda, alisema
kuwa huduma hiyo ni nzuri na rahisi inayoweza kuwanufaisha wateja na Watanzania
wote, hivyo wanapaswa kuichangamkia ili kuwaweka katika usalama wao na wa
vyombo vyao vya usafiri.
“NIKO tunajisikia faraja kubwa kushirikiana na wenzetu Bayport Financial
Services kutoa huduma bora na kiwango cha juu, hususan kwa kupitia huduma hii
mpya ya bima ya magari, tukiamini kuwa itawafanya Watanzania wote watembee
kifua mbele, maana ile presha ya kukimbiana na watu wa usalama barabarani
itakuwa imepatiwa ufumbuzi,” alisema Kigoda.
Bayport Financial Services ni taasisi ya kifedha inayotoa huduma mbalimbali za
mikopo ya fedha, mikopo ya bidhaa, bila kusahau mradi wa mikopo ya viwanja vya
Vikuruti unaoendelea na kuwafanya Watanzania watembee kifua mbele, huku taasisi
hiyo ikifanikiwa kuwa na matawi 80 Tanzania Bara, hivyo kutoa huduma bora na
kwa njia rahisi kwa kupitia matawi yao au mtandao wao
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment